UCHAMBUZI WA VIPENGELE VYA MAUDHUI


        UCHAMBUZI WA VIPENGELE VYA MAUDHUI
DHAMIRA
Dhamira nyingi zimejadiliwa katika tamthiliya hii, miongoni mwa dhamira hizo ni;
i.   Elimu ya jinsia na mahusiano.
Jamii imekumbwa na mmomonyoko mkubwa wa maadili pamoja na maradhi hatari yasiyotibika kama UKIMWI. Hivyo wazazi wanapaswa kuwaelimisha watoto wao juu ya njia sahihi za kujikinga na matatizo haya. Katika tamthiliya tunaona pande mbili, ule unaoshikilia ukale na upande unaotaka mabadiliko. Baba Anna, anawaelimisha watoto wake juu ya madhara ya kujihusisha na ngono katika umri mdogo, Anna anaelewa na anafanikiwa kukwepa vishawishi. Hali ni tofauti kwa Mama Suzi anaamini kuwapatia watoto elimu ya jinsia na mahusiano ni kuwaharibu na kuwapoteza. Anaposhauriwa kuwapatia watoto elimu hiyo anafoka,
“Huko si ndiko kunifundishia wanangu umalaya? Umfunze mwanangu habari za ngono…”
Kutokana na kutokukubali kuwapatia wanawe elimu hii, Suzi anapewa mimba na kuambukizwa UKIMWI.
          Mmomonyoko wa maadili.
Maadili hayazingatiwi tena katika jamii. Watoto kwa wakubwa wote wamepotoka. Tunaona watu wazima wakitembea na watoto wadogo, mfano Chausiku anamahusiano na mtoto mdogo Joti. Pia watoto wamejiingiza katika mahusiano ya kimapenzi, Joti anamahusiano na Suzi. Watoto hawahawa wanaangalia video za ngono bila kuogopa chochote. Katika ukurasa wa 20 Joti anasikika akiwahamasisha wenzake.
“Yaap, ukimtaka Suzi, chukua. Picha ya ngono, matusi angalia!”
Mmomonyoko huu wa maadili utaondolewa endapo watoto watapatiwa elimu.
iii.           Athari ya sayansi na teknolojia. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yameleta mabadiliko makubwa katika jamii, mfano katika tamthiliya hii, watoto wanakwenda kuangalia picha za ngono na kuwafanya waharibikiwe kifikra kwa kutamani kuigiza kile wanachokiona. Joti, mtoto kinara wa kutazama picha hizo anaambulia UKIMWI na kufa angali mtoto mdogo.
NAFASI YA MWANAMKE KATIKA TAMTHILIA YA KILIO CHETU
 . Nafasi ya mwanamke ni jumla ya mambo yote ayatendayo mwanamke katika kazi ya fasihi. Mengine huwa mazuri yanayostahili pongezi na machache huwa mabaya yanayostahili kukemewa kwa nguvu. Katika tamthiliya hii, mwanamke amechorwa kama;
-          Chombo cha starehe. Mfano Joti anamtumia Suzi kwa ajili ya kujistarehesha.
-          Asiyependa mabadiliko. Mama Suzi hataki kutoa elimu ya jinsia kwa wanaye.
-          Asiye na maadili. Suzi hana maadili, anajiingiza katika mahusiano ya kimapenzi katika umri mdogo.
-          Mwenye elimu na asiyedanganyika. Anna ana elimu ya jinsia na mahusiano, wanaume wanashindwa kumdanganya kwa pesa na maneno matamu.
           UJUMBE
i.              Asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu. Suzi na Joti hawakufunzwa vyema na wazazi wao, badala yake ulimwengu unawafunza.
ii.            Elimu ya jinsia na mahusiano itolewe kwa watoto. Elimu hii itawafanya waepuke vishawishi.
iii.           Sheria kali zitungwe dhidi ya watu wanaowalaghai watoto. Kuna watu wazima wanaowaingiza watoto katika vitendo vya kimapenzi kama Chausiku anavyomlaghai Joti. Sheria kali itungwe na isimamiwe kuwakomesha.
iv.           Wazazi wote washirikiane katika malezi ya watoto. Baba Anna na Mama Anna wanashirikiana katika malezi ya watoto wao. Matokeo bora yanaonekana.
             MIGOGORO
Migogoro iliyojitokeza ni pamoja na;
Migogoro ya wahusika
i.              Mgogoro wa Joti na Suzi.
Mgogoro huu unasababishwa na tabia ya joti kuwa na mahusiano na wasichana wengi. Suluhisho la mgogoro huu ni Joti kumuomba msamaha Suzi.
ii.            Mgogoro wa Suzi na Mama yake.
Mgogoro huu unasababishwa na mama Suzi kuvikuta vidonge vya kuzuia mimba katika sketi ya mwanaye. Suluhisho la mgogoro huu ni Mjomba kumwamuru Suzi aende ndani na mazungumzo kati ya Mjomba, Mama Suzi na majirani wengine yanaendelea.
iii.           Mgogoro kati ya Mjomba na Mama Suzi.
Chanzo cha mgogoro huu ni Mjomba kumshauri Mama Suzi ampe elimu ya jinsia na mahusiano binti yake. Mama Suzi anakataa na kusema kufanya hivyo ni kuwafundisha watoto umalaya.
iv.           Mgogoro kati ya Chausiku na Joti.
Chausiku anamlaumu Joti kuwa anamahusiano na wasichana wengine, anaendelea kulalama kuwa, hata zawadi anazompatia anawapatia wasichana wengine. Chausiku anamtisha Joti kuwa atamchoma moto yeye na visichana vyake. KICHEKO!!
Mgogoro wa nafsi
Huu ni mgogoro ambao humpata mhusika peke yake kati yake yeye na nafsi yake.
-          Suzi anapatwa na mgogoro wa nafsi pale anapopata mimba na kuambukizwa virusi vya UKIMWI. Anabaki akilia, lakini hakujilaumu mwenyewe, bali anamlaumu mama yake kwa kushindwa kumpatia elimu ya jinsia na mahusiano. Katika ukurasa wa 40, anasema,
“Mimi na Joti tungepata bahati ya kuelimishwa tusingetumbu…”
MSIMAMO
Mwandishi anamsimamo wa kimapinduzi. Katika tatizo la watoto wengi kuangamia kwa ugonjwa wa UKIMWI, anashauri elimu ya jinsia na mahusiano itolewe ili kuleta ukombozi kwa jamii.
mwandishi ametumia muundo rahisi wa moja kwa moja ambao haumchoshi msomaji wala kumchanganya.
Kufaulu kwa maudhui
-          Mwandishi amefaulu kufikisha dhamira katika jamii juu ya umuhimu wa kuwapatia watoto elimu ya jinsia na mahusiano.
-          Pia mwandishi ameifungua jamii na kuionya juu ya hatari ya sayansi na teknolojia endapo itatumiwa vibaya.
      FALSAFA
Mwandishi anaamini kuwa elimu ya jinsia na mahusiano ikitolewa kwa watoto itawasaidia kupambana na hatari ya kuambukizwa virusi vya UKIMWI.

No comments:

Post a Comment